Wanasema Uchaguzi Ukiisha Watarudi

By Wafanyabiashara wa Mtaani, Mwanza
Umri: Kati ya miaka 25–40
Kazi: Wamachinga, Wauzaji wa Mtaani
Makazi: Mwanza

Tuliondoka Kijijini Tukitafuta Riziki

Tuliondoka vijijini kwa sababu ya njaa, kwa sababu ndoto zetu zilihitaji miji mikubwa ili zitokee. Tulikuja Mwanza tukiwa na matumaini, tukiwa vijana wenye nguvu na imani kuwa tukijituma, tutajenga maisha bora. Lakini kila siku hapa mjini imekuwa kama vita ndogo. Migambo wa jiji wamekuwa kikwazo cha ndoto zetu. Wanasema wanafanya kazi yao, lakini sisi tunayaona maisha yetu yakiharibiwa kipande kwa kipande.

Kila mmoja wetu ana hadithi ya kuvunjiwa biashara, ya kupoteza mtaji, ya kurudi kuanza upya. Ndoto nyingi zimezikwa kwa sababu ya hofu, kwa sababu ya kukimbia magari ya mgambo badala ya kukimbilia wateja.

“Ofisi Ya Tano… Na Bado Narudishwa Nyuma”

Hapa mtaani tunaita vibanda vyetu “ofisi.” Kila mmoja wetu ana idadi yake ya ofisi alizopoteza. Wengine tatu, wengine nne, wengine hadi tano kama kaka yetu Nikas. Ukiamka asubuhi, huna uhakika kama jioni utakuwa na ofisi bado.

Wanakamata bidhaa zetu , viatu, nguo, matunda, kila kitu , kisha wanatuambia tulipe laki moja ili tuvipate tena. Lakini biashara yenyewe haijafika hata nusu ya hiyo hela. Ndiyo maana wengi wetu tunaishia kuanza upya kila wiki. Ni uchungu, ni aibu, lakini hatuna namna. Tunavumilia.

“Tumefukuzwa Mjini Kati Hadi Pembeni Ya Mji”

Tulikuwa tunauza mjini kati, pale ambapo watu wengi wanapita. Lakini walitutimua wakisema tunasababisha jamu. Tulihamia pembeni ya mji, lakini hata huko bado wanatufuata. Wanasema hawatutaki popote. Ni kama sisi si sehemu ya mji huu.

Kuna siku tunasubiri hadi jioni saa 11 ndipo tunafungua biashara. Wakati wengine wanafunga maduka yao, sisi ndio tunaanza kuuza. Tunauza gizani, tukiogopa magari ya mgambo. Wakati mwingine tunalipa kodi, lakini bado wanakuja. Hata wakituona tunakimbia na mabango mgongoni, hawasikii huruma.

“Tukiwaza Familia, Tunahisi Kuchanganyikiwa”

Kila mmoja wetu ana familia nyuma yake — watoto, wake, wazazi. Tunajua kwamba tukirudi nyumbani mikono mitupu, hakuna chakula. Wengine wetu tunatembea kwa miguu kutoka mbali, tukiwa hatujala, tukiwa na njaa lakini na tunapambana.

Mara nyingi tunajikuta tukiwa kimya, tukiwa tumekaa kando ya barabara tukitazama mabaki ya bidhaa zilizoanguka, tukijiuliza: je, haya maisha yatabadilika? Kuna wakati mtu anahisi kuchanganyikiwa. Lakini bado kesho tunarudi tena, kwa sababu hatuwezi kuacha familia zetu njaa.

“Wanasema Watarudi Baada ya Uchaguzi Kupita”

Mwezi wa tano mwaka jana, tulianza kuona tofauti. Migambo ilipungua. Biashara zetu zikaanza kupumua tena. Wengine wetu tukaanza kupata faida kidogo. Wengine tu kafurahia kurudi kazini bila kukimbia. Lakini tukasikia uvumi eti baada ya uchaguzi, watarudi.

Sasa tunaishi kwa hofu. Tunafanya kazi, lakini mioyo yetu ina hofu ile ile. Tukiona gari la manispaa likipita, mioyo inaruka. Tunajiuliza: “Je, leo ndio mwisho wa ofisi hii tena?” Wengine wetu tumeamua kuomba sana Mungu awazuie wasirudi, maana tukianza upya tena, wengi wetu tutapoteza kabisa.

“Tunajipa Moyo, hatuachi Kujaribu”

Hapa mtaani, kila mmoja wetu ana kauli moja: jipe moyo, usikate tamaa. Ni kauli ya maisha. Tumeipamba kwenye mabanda yetu, kwenye mioyo yetu. Tunajua siku moja tutavuka.

Tunaamka alfajiri, tunafanya kazi hadi usiku. Tunasaidiana, tunalindana. Tunataka watoto wetu waone kuwa bidii bado inalipa. Hata kama leo tunauza chini ya kivuli, tunajua ipo siku tutakuwa na maduka yetu.

Tunapambana si kwa ajili yetu tu, bali kwa ajili ya vizazi vijavyo. Ili waseme: “wale wamachinga wa Mwanza walipigania haki yao ya kuishi mjini.”

Tunaishi, Tunapambana, Tunatumaini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *