Nilitaka Kuwa Rubani, Nikawa Daktari Kiganjani

Jina: Dr. Ayoub Msalilwa
Umri: 35
Kazi: Daktari na Mwanzilishi wa Daktari Kiganjani
Makazi: Dar es Salaam, Tanzania

Swali: Je,Ulijua tangu mwanzo kwamba utakuwa daktari?

Dr. Ayoub: Hapana. Nilipokuwa mdogo, nilitaka kuwa rubani. Nilikuwa na ndoto ya kupaa. Lakini maisha, kama yalivyo kwa wengi wetu, yalibadilisha mwelekeo.

Dr. Ayoub: Nikiwa darasa la tano, mdogo wangu wa kike aliungua vibaya kwa maji ya moto alipokuwa akicheza. Niliporudi kutoka shule, nikamkuta hospitalini Iringa. Siku ya tatu, alipoteza maisha. Alikuwa na miaka mitatu tu. Niliona kifo chake kwa macho yangu.

Nilihisi kama dunia imeninyang’anya kitu ambacho singewezakurudisha. Na mbaya zaidi, niliona hakupata huduma ya msingi kabisa. Hakuna aliyemwekea dripu, hakuna aliyemgusa kwa haraka. Nilipofundishwa baadaye kwenye somo la Biology kuhusu maji mwilini, nilijua mdogo wangu hakutakiwa kufa. Alikufa kwa sababu ya huduma duni.
Hapo ndipo nilipoapa: “Nitakuwa daktari. Nitaokoa maisha mengine kama yake.”

Swali : Ulianza lini kujiona kama daktari?

Dr. Ayoub: Nilianza shule. Nilikuwa najifanya daktari kwenye michezo ya watoto. Nilikata plastiki, nikatengeneza vifaa vya majaribio, nikiwa na ‘patients’ wangu wa kufikirika. Wakanipa jina ‘daktari’ kabla sijawa mmoja kweli.

Miaka ilipita, ndoto ile ikakua. Baada ya masomo, hatimaye akawa daktari halisi lakini si yule aliyekaa ofisini tu.

Dr. Ayoub: Nilijikita zaidi kwenye huduma za mama na mtoto. Nilihisi nafanya jambo ambalo lingemfanya mdogo wangu atabasamu huko alipo. Lakini bado nilihisi kuna pengo kubwa.

Hapa Tanzania, daktari mmoja anaweza kuona wagonjwa zaidi ya elfu nne kwa mwaka. Uingereza, wanaona mia mbili tu. Unafikiri kweli unaweza kumsaidia mtu kwa dakika tano za mazungumzo? Nilianza kujiuliza: “Ninawezaje kufika mbali zaidi ya ofisi yangu?”

Swali: Kuna tukio lolote lililokugusa zaidi baada ya kuwa daktari?

Dr. Ayoub: Ndiyo. Nilipooa, na tukapata mtoto, marafiki wawili tuliokuwa nao walipoteza watoto wao mmoja akiwa tumboni, mwingine mara tu baada ya kuzaliwa. Iliniuma. Nilijiuliza, ‘Kwa nini mimi nilipata, na wao walipoteza?’

Dr. Ayoub: Nilihisi wajibu mpya wa kugawana elimu. Nilianza vipindi vya redio kuhusu afya ya mama. Nilizungumza kuhusu ujauzito, chanjo, lishe. Baadaye nikaanza kurekodi video na kuzisambaza mtandaoni. Nilitaka kila mtu awe na daktari mkononi hivyo Daktari Kiganjani alizaliwa.

Swali: Kwa nini jina Daktari Kiganjani?

Dr. Ayoub: Awali nilitaka kuiita Daktari Wangu, lakini jina lilikuwa limechukuliwa. Nilipoona tunafikia watu wengi kupitia simu zao, nikaona bora liitwe Daktari Kiganjani daktari aliye mkononi mwako.

Swali: Na tangu hapo?

Dr. Ayoub: Tumekuwa zaidi ya miaka minne. Video zetu zimefikiwa na watu zaidi ya milioni nne. Lakini siyo idadi ninayoangalia. Ni hadithi za mtu mmoja mmoja.

Dr. Ayoub: Alinipigia simu baada ya kuona video yetu. Niliposikia dalili za mtoto wake, nilitambua ni hatari. Nikamwambia aache kupoteza muda, akimbize mtoto hospitali. Baada ya siku tatu alinipigia simu akisema, “Daktari, uliniokoa.” Nililia kimya kimya.

Swali: Umewahi kuona matokeo ya kazi yako kwa macho?

Dr. Ayoub: Siku moja nilikuwa barabarani, nikasikia mtu akimwambia rafiki yake: “Haya maji unatakiwa unywe hivi daktari mmoja anasema hivyo.” Kisha akabonyeza simu yake, nikasikia sauti yangu. Nilihisi faraja kubwa.

Swali: Imekua zaidi ya ulivyotarajia, eeh?

Dr. Ayoub: Kabisa. Siku moja nilitoa kipindi fulani, nikapokea simu 212 kwa siku moja. Watu walitaka kuelewa zaidi, kuuliza na kujifunza. Nilijua basi hii ndiyo maana ya kuwa daktari kwa watu, si kwaajili ya huduma ya hospitali pekee.

Dr. Ayoub: Kuna siku mwandishi wa redio alikata tamaa. Madaktari wote alowaita kwaajiri ya mahojiano walikataa. Alikuwa karibu kufukuzwa kazi. Rafiki yake akanifuata kanisani. Nikawasha gari, nikaenda redioni bila maandalizi. Nilimkuta amekaa na machozi. Tulianza kipindi. Simu zilianza kupigwa. Watu waliguswa, mtoto aliyenusurika baada ya mama yake kusikia ushauri wake kwenye kipindi hicho mtoto aliyekuwa karibu kupoteza mkono kwa kuungua.

Swali: Unaposema Daktari Kiganjani ni urithi, unamaanisha nini?

Dr. Ayoub: Naamini kila video, kila sauti, ni urithi wa vizazi vijavyo. Daktari Kiganjani sio mradi wangu tu, ni maktaba ya elimu ya afya kwa Watanzania. Maono yangu ni kuona maudhui ninayotengeneza yakifikitumika hospitalini, redioni na hata wenye mitaala ya afya kini zaidi sana kuwafikia wale ambao mkono wa daktari hauwezi kufika.

Swali: Ujumbe wako wa mwisho ni upi?

Dr. Ayoub: Siwezi kubadilisha dunia nzima. Lakini nikimsaidia mtu mmoja, huyo mtu mmoja anaweza kumsaidia mwingine. Hivyo ndivyo dunia inavyobadilika kwa msaada mmoja unaoendelea kwa watu wengine.

Dr. Ayoub: Mimi naamini katika ujipa moyo na kutokukata tamaa. Huo moyo ndio uliofanya maumivu ya msiba wa mdogo wangu yazaliwe upya kama tumaini. Ndiyo uliogeuza ndoto ya urubani kuwa urubani wa maisha kupitia tiba, elimu, na sauti. “Ndiyo maana niliishia kuwa daktari kiganjani si kwa bahati, bali kwa wito.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *