Hapo zamani za kale, kulikuwa na kijana mmoja jina lake Kennedy. Kijana huyu aliishi Morogoro, mji wenye milima ya kijani kibichi na mashamba ya mahindi na maharage. Alikuwa mtoto wa kiume pekee katika familia yake, akiwa na dada zake wawili. Baba yake na mama yake walikuwa wakulima wa kawaida, wakilima mazao yaliyotosheleza familia yao, na Mungu alikuwa akiwabariki.
Kennedy alifanya vizuri shuleni, lakini baada ya kidato cha nne, hakufanikiwa kwenda kidato cha tano. Akabaki nyumbani akisaidia wazazi wake kilimo na ufugaji. Miaka miwili ikapita, kijana akiwa bado hajafikiri zaidi ya mashamba na mifugo.
Siku moja, jambo la tofauti lilitokea wa Kennedy.
Rafiki wa baba yake akaja kutoka Dar es Salaam, mji mkubwa wenye kelele na pesa. Walipokuwa wanaunywa chai na kupiga stori, rafiki huyo akauliza, “Kijana yako yuko wapi?” Baba akamweleza, “Yuko nyumbani, anasaidia shamba.” Rafiki akasema, “Kuna mtu Dar, anaishi Ulaya. Anatafuta kijana wa kuangalia nyumba yake. Kijana wako yuko vizuri na ni mwaminifu. Hebu umpeleke.”
Baba akamwambia Kennedy. Kwanza kijana akakataa. Aliogopa jiji, aliogopa maisha mapya. Lakini akawaza: “Labda nitapata pesa, nitaweza kuanza biashara.”
Akapokea nauli. Safari ikaanza.
Ilikuwa Jumapili asubuhi. Mvua ilikuwa inanyesha pole pole, baridi ilikuwa kali. Kennedy akasafiri kwa basi kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam. Alipofika, alishuka Kimara Temboni, sehemu yenye makazi na watu wengi. Akampigia mwenyeji wake simu. Mwenyeji akaja kumchukua.
Nyumba ile! Eeh, nyumba kubwa, yenye bustani safi ndani na nje, maua ya kila aina. Kennedy akaambiwa kazi yake ni kuangalia nyumba, kufanya usafi, na kutunza bustani. Boss wake na familia yake waliondoka kwenda Ulaya, wakabaki huko kwa muda mrefu.
Kennedy akakaa pale miaka sita. Sita kamili! Akafanya kazi kwa uaminifu mkubwa, hata hakuiba japo kalamu moja. Boss wake akamwamini, akamsaidia anapohitaji, hata nyumbani akituma pesa. Kijana akawa na akiba kidogo kidogo.
Siku moja, Kennedy akaamua. Akasema, “Mimi nataka kuanza biashara yangu.”
Boss wake na baba yake wakasikitika sana. Wakasema, “Usitoke, kaa hapa.” Lakini Kennedy alikuwa ameamua. Mwishowe, wakampa baraka zao.
Kennedy akahamia Mbezi, sehemu ya vibanda na biashara ndogo ndogo. Akapanga chumba kimoja tu, ghetto rahisi. Akanunua kibanda cha chuma chenye matairi, akaweka bidhaa ndogo ndogo ,sabuni, unga, sukari na uwakala wa kutuma na kupokea pesa.
Kibanda chake kilikuwa jirani na kijiwe cha bodaboda. Madereva wengi wakamjua. Wengine wakamwamini sana hadi wakamwazima pikipiki zao aende Kariakoo kufuata mizigo. Kennedy alifanya kazi kwa bidii. Biashara ikawa inakwenda vizuri.
Lakini kama ilivyo katika hadithi zote shida ilikuja ghafla!!
Siku moja jioni, mama mmoja akaja kwa Kennedy. Akatoa pesa. Baadaye akapanda bodaboda ya dereva mmoja na akaondoka. Kennedy akaendelea na shughuli zake kama kawaida.
Kesho yake, usiku anapanga kufunga kibanda, polisi wawili wakaja. Walijitambulisha na kusema, “Tunamtafuta yule bodaboda. Alisafirisha mama fulani, akambaka na kumuibia. Wewe unamjua?”
Kennedy akasema, “Sijui jina lake, najua sura tu.”
Polisi wakasema, “Ukishindwa kumtaja, tunaondoka na wewe.”
Kennedy alijaribu kuwaeleza, Simjui, Simjui! Lakini polisi hawakusikiliza. Wakamchukua. Akafunga kibanda chake, akaenda nao kituo cha polisi Gogoni.
Hapo ndipo, safari yake ya giza ilianza.
Kennedy aliingia ndani. Akakabidhi simu yake na vitu vyake vyote. Alipoingia ndani ya selo, hakuamini macho yake. Aliwaza: “Mimi? Nilmefika vipi hapa?”
Mwanzoni alikuwa na uchungu, hasira, na hofu. Alikosa mtu wa kumpigia simu, alikosa msaada. Hakujua kesi yake, hakujua lini atapanda mahakamani. Siku zikapita. Wiki zikapita. Miezi ikapita—moja, mbili, tatu, nne.
Lakini, kama desturi ya watu wema Kennedy akaanza kushirikiana na wenzake ndani. Mtu akiletewa chakula, wakagawana. Wakawa kama familia ndogo ndani ya ukuta wa mahabusu.
Siku zote Kennedy alikuwa akijiuliza, “Je, kweli wanyonge hawana sauti?”
Wakati Kennedy alipokuwa akifanya kazi kwa boss wake wa zamani, alikuwa anajuana na wafanyakazi wa baba yake boss, mzee mwenye mashamba na mifugo. Mmoja wa wafanyakazi wake aliitwa Mayao.
Siku moja, ndugu yake Mayao naye alikamatwa na kufikishwa pale kituoni. Mayao alienda kumtembelea. Alipofika pale, akamuona Kennedy! Akashangaa sana. “Wewe vipi tena hapa?”
Kennedy akasema kwa sauti ya unyonge, “Tafadhali, waambie baba na boss wangu. Nimelala ndani mwezi wa nne huu sasa . Sina msaada.”
Mayao akaenda haraka. Akamwambia baba—yule mzee mwenye mashamba.
Kesho yake, baba akaja. Ni mtu mwenye ushawishi na hela. Akaongea na askari. Akaweka pesa mahali fulani. Na Kennedy akatoka.
Baba akamwambia baadaye, “Yule mama aliyelalamika, ni mke wa mtu mwenye cheo na nguvu. Ndio maana walikuchukua bila haki.”
Kennedy alirudi nyumbani kwa mzee. Hali yake kiafya na kiakili ilikuwa imeyumba. Akaamua kurudi kwa boss wake wa zamani, akaendelea na kazi ya bustani. Alifanya kazi kwa bidii miaka miwili, hadi alipojihisi tayari kuanza upya.
Lakini cha kuskitisha!—kibanda chake cha biashara kilikuwa kimeibiwa. Chumba alichopanga, mwenye nyumba alikuwa amevunja kitasa chake, akauza vitu vyake, akampangisha mtu mwingine. Kennedy alikuwa amepoteza kila kitu.
Lakini kijana hakukata tamaa. Alianza upya. Leo, ana kibanda kingine cha biashara kinachofanya vizuri, na anaendelea na kazi ya bustani kama mtaalamu kwa watu mbalimbali.
Kennedy alisema kitu kimoja: “Nilijifunza kitu kimoja—sio kila aliye jela ana hatia. Pesa na ushawishi vinaweza kumuumiza asiye na sauti. Lakini Tanzania hii, bado naamini: unaweza kuanguka, ukaamka tena.”
Hadithi yetu imeishia hapo,
Hadithi hii imesimuliwa na Kennedy Masimbu na kuhaririwa na Primi F Fidelis, Juni
2025,