Ushairi wa Gifted Son
Umri: 29 | Msanii wa Hip Hop | Dodoma
Nilizaliwa Surprise,
pale Chadulu,
si mahali pa shangwe,
bali mahali pa mshangao:
unawezaje kuishi hapa na kubaki hai?
Mama alikuwa baba,
mtaa ulikuwa mwalimu,
pombe ilikuwa biashara,
na mimi nilikuwa mtoto,
ndoto zikiwa bado mbali,
lakini maisha yakiwa karibu sana.
Komoni. Kangara. Choya.
Majina haya si dawa,
lakini ni chakula cha familia yangu.
Mama na mabibi,
waliuza ili tuwe hai,
na mimi, mtoto mdogo,
nilikulia mgongoni,
nikiwa sehemu ya biashara hiyo.
Nililia,
wakanishushwa.
Wakanitafunia pombe kidogo,
ili nipate usingizi.
Hii si hadithi ya kubuniwa.
Hii ni ukweli wa Chadulu.
Wateja walinijua,
walinipenda,
walinipa pipi,
walinituma sigara,
nikawashie,
mtoto mdogo nikipiga pafu,
ili sigara ifike ikiwaka.
Hiyo ilikuwa chekechea yangu.
Mafunzo ya mtaa, si shule.
Mtaa ulikuwa darasa,
sigara ilikuwa kalamu,
na pombe ilikuwa ink-
niliandika maisha yangu kwa damu.
Lakini mama aliona.
Kuna wakati mama huona zaidi ya wote:
Mtoto wangu anakufa pole pole.
Akaacha biashara.
Tukahama.
Nikapata nafasi ya kuondokana na moto huo.
Mimi ni kijana niliyeponyoka kwenye moto,
si kwa sababu nilikuwa hodari,
bali kwa sababu mama alikuwa na nguvu za kuponyoka nami.
Baba alikuwa in and out.
Si ndani, si nje.
Alikuwa kama kivuli,
unakiona mara moja,
halafu kinatoroka.
Hakuwahi kuwa sehemu ya maisha yangu kikamilifu.
Hakuwahi kuniambia kwa nini aliachana na mama.
Mama akaniambia tu:
“Ukishamkera mama yako, nenda kamtafute babako.”
Nilikua bila father figure.
Naamini kama angekuwepo,
labda singeacha madrasa,
labda singeingia mtaani haraka hivyo.
Mama alijitahidi,
Aki vile, alijitahidi!
Lakini kuna vitu vinahitaji mkono wa baba,
kuna sauti ya baba ya kusema:
“Hii si njia yako.”
Sauti hiyo haikuwepo.
Kwa hiyo mtaa ukawa baba wangu.
Mwaka 2014,
nilikuwa studio pamoja na Bin Laden,
Roma, na wasanii wengine.
Kulitokea kutoelewana pale studio—
nilikasirika, nikajiondoa.
Saa chache baadaye,
nikasikia taarifa—
Roma na wengine wametekwa.
likuwa ni studio ile ile.
Nikasema ndani yangu:
Kumbe kuondoka pale ilikuwa neema ya Mungu.
Leo hii, naendelea kuishi,
kusema,
na kuimba,
kwa ajili ya wale ambao hawakuweza.
Maisha ni studio,
na wewe unachagua mistari yako.
Mimi nilichagua kuendelea.
Chadulu Mentality,
si tu albamu,
ni msimamo wa maisha.
Kwa kijana kutokea Chadulu na kufanikiwa,
ni kama miujiza.
Ukifanikiwa Chadulu,
basi unaweza kufanikiwa popote.
Mistari yangu inazungumzia maisha halisi,
kule tulipotoka,
tulichopitia,
na matumaini ya kesho.
Wimbo wangu Ndoto ulifika mbali.
Watu walinipigia simu,
watu wa kila aina,
hata waheshimiwa,
wakasema:
“Mistari ile imegusa maisha yangu.”
Hapo ndipo nilijua:
Sauti ya mtaa inaweza kuwa uponyaji kwa wengi.
Nilipoanzia sina hata shilingi 100.
Nilipoanzia na maumivu zaidi ya 100.
Lakini kuanzia bila kitu,
ni kuwa na kila kitu cha kupoteza,
maana huna cha kupoteza.
Kwa hiyo unacheza kwa moyo wote,
unaimba kwa sauti yote,
unaandika kwa damu yote.
Sasa ninaimba,
si kwa ajili ya pesa tu,
bali kwa ajili ya kijana yule wa Surprise,
ambaye alikulia mgongoni,
akilala kwa pombe,
akiwa anajua tu sigara na matope.
Ninaimba kwa ajili yake,
ili ajue:
Unaweza kutoka Surprise na kufanikiwa.
Unaweza kuwa orphan wa baba, lakini usifukuzwe na ndoto.
Unaweza kuwa mtoto wa pombe, lakini usiwe mnywa wa maisha yaliyopotea.
Mama alikuwa baba,
mtaa ulikuwa mwalimu,
muziki ukawa uponyaji,
na mimi nikawa shahidi,
kwamba hata kule Chadulu,
kuna vijana wanaoandika historia.
Sina shilingi 100 za mwanzo,
lakini nina sauti moja,
na sauti hiyo inazungumza kwa ajili ya wengi.
Kwa wale waliopotea studio,
kwa wale waliotekwa mtaani,
kwa wale ambao baba hawakuwapo,
kwa wale ambao mama alikuwa kila kitu,
Mimi ni sauti yenu.
Mimi ni Gifted Son.
Na hii ni hadithi yetu.
Ushairi umeandikwa kwa heshima ya Gifted Son na wale wote wanaoimba kutoka kwenye
matope.
Mahojiano na ushairi na: Fredrick Aloyce , 2025