Dondosha Dude

Na Kasongo
Umri: 40
Asili : Tunduma – Mangulueni

“Nilikuwa Tayari Kumpiga Mama Kisu”

Sikumbuki sura ya baba yangu. Alifariki nikiwa na miezi miwili tu. Mama alinileta Tanzania kutoka Zambia nikiwa bado mchanga, tukaanza maisha Tunduma kwenye majengo ya Mangulueni. Huko ndipo nilikulia, nikiwa mtoto wa mwisho katika familia iliyoishi vipande vipande. Ndugu zangu walitawanyika, kila mmoja akaenda kuishi kwa ndugu, Mimi nikaachwa na mama pekee yake, Mama ndiye kila kitu kwangu. Lakini hata yeye hakujua maisha halisi niliyopitia.

Nilianza kuvuta bangi darasa la tatu tulikuwa watatu mimi na washikaji wangu wa shule. Kila siku tukimaliza masomo ya asubuhi, tunahepa shule, tunaingia kwenye bustani ya hospitali ya serikali pale Tunduma, tunajificha katikati ya majani tunavuta. Bangi tulikuwa tunanunua klabuni kwa jamaa mmoja shilingi mia tatu tu.

Darasani nilikuwa kichwa, lakini mtukutu kuliko wote Nilikuwa na maisha mawili mmoja wa shule, mwingine wa mtaani Marafiki wa mtaani walikuwa tofauti na washuleni Na walipogundua mimi navuta, wazazi wao wakaanza kuwakataza kuniendea: “Usicheze na mtoto wa fulani.” Hapo ndipo nilianza kujitenga, kuhama mitaa, kutafuta makundi mengine, mitaa mingine na tabia zikaendelea kuharibika.

“Twende nikakufundishe kazi”

Nilianza kukutana na watu wakubwa wezi, wakaba, vijana waliokomaa kwenye uhalifu.Nikiwa darasa la nne tayari nilikuwa natumika. Kuna siku nilichelewa kurudi nyumbani, nikalala kwa brother mmoja ambaye alikuwa jambazi sugu. Usiku akaamka, akaniambia, “Mdogo wangu leo kazi ipo, twende kazini.” Nikakubali, tukatoka, nikapewa maagizo: “Simama hapa. Ukiona mtu anapita, sema umepotea nyumbani.” Nilifuata maelekezo. Alinichukua dada mmoja ambaye aliniamini na kutaka kunisaidia ili nilale kwake usiku huo na kesho kunipeleka polisi kwa msaada lakini usiku huohuo tulimuibia tv,deki na radio,Ndiyo kazi niliyofundishwa.

Nilizidi kuwa sugu. Nikaanza kukaba wanawake, watoto wa kike, nikiamini mwanaume siwezi kumvaa. Ilikuwa kawaida kwangu kuwa mtaani usiku naruka ukuta, napanda paa, natoroka nyumbani. Nikakutana na dondosha dude.

“Dondosha Dude”

Dondosha dude ni mchezo wa ujanja na wizi unaofanyika mpakani mwa Tunduma. Tunatumia dola feki, magazeti yaliyofungwa kama hela, tunamdondoshea abiria kutoka nchi jirani, anafikiri kapata bahati. Tunamchukua sehemu tulivu inaitwa Danida tunamvizia, tunampiga, tunampora kila kitu. Baadhi waliuawa kule ndio mchezo pia ambao umeua rafiki zangu wengi.

Nilishawahi kufikiria hata kumpiga mama yangu kisu si kwa sababu alinifanyia ubaya, bali kwa sababu bangi, hasira, na tamaa zilikuwa zimeniua ndani.

Nilifika hatua nikauza sigara na bangi shuleni. Nikawa maarufu kuliko walimu. Nilikuwa naweza kuingia darasani saa moja, kutoka saa tatu na kwenda zangu forest Huko tunakutana na wanafunzi wa kike na wakiume nawauzia tunavuta.

“Unakubalije unafukuzwa kizembe”

Siku hiyo mwalimu mkuu aliniambia nisiendelee kwa sababu sikufanya mtihani wa kwanza wa form 2 akaniambia nikitaka kuendelea na shule basi urudie darasa Niliumia Lakini ndani ya nafsi nilijua nilishakata tamaa nikaona bora tu niache tu shule nilifukuzwa darasani nikaondoka nikaenda zangu sasa mtaani jamaa wangu nakumbuka aliniambiaga wewe ni mjinga sana mwanangu yaani kile kimwalimu kinakufukuza na unakubali hata kama umefukuzwa umekubali ungekipiga kwanza.

Nilijiunga na kundi la watu wazima. Tukaanza mazoezi – si mazoezi ya afya, bali ya nguvu kwa ajili ya kazi za usiku: ukabaji, kuvamia nyumba, kuvunja maduka. Nikaingia kwenye kundi la kuiba mafuta, simu, redio, deki, kupeleka Zambia. Nilitoboa kuta, niliingia kwenye nyumba za watu usiku, niliiba lakini roho haikuwahi kushiba.

Nakumbuka siku moja Krismasi, nilikunywa pombe hadi nikazimia. Nilivaa kiatu cheupe, jeans nyeusi, na T-shirt nyeupe. Sikutambua nilikuwa karibu kufa. Brother mmoja akanichukua kunipeleka kwa mtu akalale. Niliamshwa usiku, watu wakaniita mwizi. Nililia Niliomba Nikatambuliwa na kuachwa. Lakini haikunitosha Nilirudi mtaani.

“Brother ni wewe?!”

Niliishi miaka mitano Dar es Salaam baada ya brother kunichukua Nikaanza kujitambua taratibu Lakini bado, ndani yangu, kulikuwa na ndoto ya hela na hiyo ilibaki sumu.Nilirejea Tunduma Siku moja nikiwa na mpenzi wangu tukitoka klabu usiku, tulikutana na kundi la vijana zaidi ya 20, wamebeba mapanga, tochi, silaha za kienyeji. Niliwaangalia, waliniangalia. Wakagundua mimi ni nani. Nikasalimiwa: “ah Brother, kuwakagua ni madogo ambao niliwachaga wakiwa wadogo sana kwa hiyo bila kufahamika wangenidhuru wao walisema sisi tunachukua vyetu tunachukua mali hatukill basi tulimpeleka yule mwanamke wangu akalale alafu sasa mimi nikaingia mtaani nasemaga dar haina wizi .

“Naingia nachukua mali”

nakumbuka kuna duka ambalo tulichukua kamba tukachana bati hata kama ina bodi tunachana unaifunga kamba unashuka na ile kamba kama komando au mnaweza mkachimba au kutoboa ukuta na hiyo kazi inafanyika kipindi cha mvua, Unajua kipindi cha mvua mvua za usiku zile zinapiga sana kelele inapopiga batii mi nachimba huko naondoka na kitu.

“Niliamua Kubadilika”

Baada ya kurudi Dar, nilipokea simu: rafiki yangu yule ambaye tulikuwa tunapanga naye kuingia kwenye kazi ya kuuza madawa, kudondosha dude, kufanya ukabaji mkubwa ameuawa. Waliokuwa naye wote wamekufa au wako jela. Nikaangalia maisha yangu. Nikasema: “Mimi nilipaswa kuwa kwenye hiyo orodha”, Hapo ndipo mabadiliko yalipoanza.

Nilianza kujiweka mbali na mitandao ya kihalifu. Nikapunguza bangi. Nikajifua tena mazoezi, lakini si kwa ajili ya kupiga watu kwa ajili ya afya. Nikaanza kujitafuta upya. Wakati rafiki zangu wanapiga kazi za kihalifu, mimi nalia kimya Wakati wengine wanagawana mamilioni, mimi najifungia, najifikiria.

Nisingekuwa na brother yangu, labda ningekufa. Mama hakuwahi kujua yote Sikumwambia hadi baadaye.

Mhariri/Mahojiano: Neema Mikomangwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *