Imeandikwa na: Frank Selebwa
Umri: 31
Kazi: Dereva Bajaji
Makazi: Dar es Salaam, Tanzania
Mpendwa Tanzania ya Kesho,
Ninakuandikia barua hii nikiwa ndani ya bajaji yangu, nikisubiri abiria kwenye jua la mchana wa Dar es Salaam. Barabara zimenifundisha mengi kuliko vitabu. Vumbi, kelele, na harufu ya petroli vimekuwa walimu wangu wa maisha. Na leo, napenda kukuambia ukweli mdogo ambao labda bado haujabadilika katika wakati wako: tulifundishwa kubuni kwa kichwa.
Nakumbuka siku ya mwisho chuoni, VETA. Mwalimu wetu alisema, “Tubuni tu kwa kichwa.” Tulikuwa tunasoma PLC- teknolojia ya viwanda , bila kifaa, bila maabara, bila
hata picha ya kile tunachojifunza. Tulikariri maneno , na tukapewa vyeti vya maarifa ambavyo hatukuyaona. Nilihisi kama nimefundishwa kuota, si kufanya.
Nilipomaliza, nikaenda ofisini kutafuta leseni. Afisa mmoja akanitazama na kuniambia: “Dereva huyu ni Mkigoma, labda si raia.” Faili langu likafungwa. Nikarudi kijijini,ilibidi nirudi tena mjini, mara tatu, mara nne, hadi nikapata karatasi ya leseni. Hapo ndipo nilijua kua hapa nchini, kutaka kufanikiwa ni safari ndefu, si kwa sababu hatuwezi, bali kwa sababu haturuhusiwi kufikiri zaidi ya mipaka tuliyopewa.
Ndugu Tanzania ya Kesho,
Sijui kama bado una watoto wanaosoma kwa kukariri vitabu, au kama sasa wanafunzi wanagusa vitu, wanauliza maswali, wanajaribu. Lakini mimi wa sasa ninajua hili: elimu yetu haikukusudiwa kutufanya huru, bali kutufanya watulivu. Ukiuliza kwa nini, unaonekana mkorofi. Ukihoji maamuzi ya wakubwa, unasemwa unapinga maendeleo. Tumefundishwa kukubali, si kufikiri. Na hiyo ndiyo siri kubwa ya mfumo unaotawala kimya kimya mfumo unaoogopa watu wanaouliza.
Mpendwa mimi wa Kesho,
Ninaendesha bajaji, lakini ninafikiria nchi. Kila safari ninapopita Kariakoo, Ubungo, au Magomeni, naona uso wa Tanzania. Ni macho ya watu waliochoka lakini bado wanatabasamu. Ni mioyo iliyokubali hali ilivyo, kwa sababu haijui inaweza kuwa tofauti. Amani yetu ni ya ajabu amani ya kimya. Watu hawaulizi, kwa sababu waliambiwa amani ni kutohoji. Lakini mimi najua: amani ya ujinga haiwezi kujenga taifa.
Ninapokuwa usiku kwenye bajaji yangu, taa za magari zikimetameta, ninajiuliza swali moja tu:
Kama Tanzania ingeandika barua kwa nafsi yake ya baadaye, ingesema nini?
Labda ingesema hivi:
“Nilikuwa na kila kitu madini, ardhi, watu wenye akili na mikono. Lakini niliwafundisha kubuni kwa kichwa badala ya kutumia mikono. Niliwafundisha kukubali badala ya kufikiri. Niliwazuia waulize kwa nini, na nikaita hiyo nidhamu. Nilijenga shule zisizo na vifaa, na nikaita hayo maendeleo. Nililinda amani ya kimya, nikaiita mafanikio. Lakini ndani, nilikufa polepole.”
Labda pia ingeongeza:
“Najua sasa, elimu ya kweli ni ile inayowasha akili, si inayozima. Nchi haiwezi kuamka ikiwa watoto wake wanalala darasani. Najua mabadiliko hayawezi kuletwa na viongozi pekee, bali na watu wanaohoji, wanaojaribu, wanaovumbua.”
Mpendwa miimi wa Kesho,
Ninaomba usikate tamaa. Wimbo wangu wa kila siku ni ule wa Darassa na Ben Paul “Sikati tamaa, life is hard.” Ninauimba nikikwepa mashimo ya barabara, nikijiambia kesho inaweza kuwa bora. Siyo kwa sababu nimeona ishara, bali kwa sababu bila matumaini, hatuna kitu cha kuishi nacho. Elimu itakapokuwa huru, akili zitafunguliwa, na watoto watapewa nafasi ya kuuliza kwa nini hivi na si vile, siku hiyo Tanzania itakuwa imejijibu barua yake yenyewe.
Ndugu Tanzania ya Kesho,
Kama utanisikia, tafadhali sema na watoto wako maneno haya:
“Usiogope kuuliza. Usikubali kukubali tu. Fikiri. Jaribu. Fanya.”
Hayo ndiyo maneno yatakayogeuza taifa hili kutoka nchi ya vyeti kuwa nchi ya ufahamu.
Kwa sasa, nitaendelea kuendesha bajaji yangu, nikipeleka watu sehemu mbalimbali, nikitazama barabara za mji huu zikipumua polepole. Na kila moshi ninaoupumua, ninajua , mimi ni sehemu ya Tanzania inayotafuta jibu lake.
Wako kwa matumaini,
Frank Selebwa
Dereva Bajaji, Mwananchi wa Tanzania