Barua kwa Imma: Samahani kwa Kukaa Kimya

Kwa: Emmanuel (Imma) — Huko Ulipo
Kutoka: Elisante Ephraim
Tarehe: Oktoba 17, 2025

Rafiki yangu Imma,

Sijui kama barua hii itakufikia huko ulipo. Sijui kama kuna njia ya maneno yangu kukupata kule mbinguni, au popote roho zetu zinapoenda baada ya kuacha dunia hii. Lakini leo, baada ya miaka mingi ya kubeba uzito huu kifuani, lazima niandike. Lazima nikwambie kile ambacho ningelipaswa kusema kabla ya siku ile, ile siku ambayo uliniacha katikati ya barabara, ulipopigwa na wananchi wenye hasira kali, ulipotoka duniani ukiwa bado ni mtoto.

Unakumbuka maisha yetu? Kimandolu? Mchana tulikuwa watoto tu wa kawaida mtaani, magoti yamejaa vumbi, viatu vimechanika, tukichezea vumbi vichochoroni. Usiku tulikuwa watoto safi nyumbani. Hatukua na maisha ya juu sana kama wengine, lakini tulikuwa na familia. Mimi nilikuwa na wazazi, na hata pale tulipokuwa na shida, kulikuwa na mtu wa kutegemea.

Lakini wewe, Imma? Hukuwa na hata kile kidogo tulichokuwa nacho sisi. Madaftari—hukuwa nayo. Sare za shule—hukuwa nazo. Msaada wowote kutoka kwa wazazi? Pia haukua nao. Ilikuwa ngumu kwako, lakini wewe ulibaki kuwa mmoja wa marafiki wa kweli kabisa niliowahi kuwa nao maishani mwangu.

Siku Ile Nilikosa Kuokoa Maisha Yako

Nakumbuka kipindi cha darasa la tano au sita hapo, tulikuwa bega kwa bega. Kila siku nikitoka shuleni tunakutana barabarani, tunacheza pamoja mpaka baadae kabisa. Lakini siku moja, nilirudi nyumbani kutoka shule na hapo Imma, nilikukuta barabarani. Ulikuwa umelala pale, mwili wako umeumia, watu wakizunguka. Wananchi walikuwa wamekupiga kwa hasira kali.

Sikuweza kuhisi chochote. Sikuweza kulia. Nilikuwa tu nimesimama pale, nikitazama maiti yako, nikijiuliza: “Kwa nini? Kwa nini Imma?”

Unajua nini Imma, Kilichoniuma zaidi sio tu kwamba uliondoka. Ni kwamba nilijua! Nilijua kama ningesema kwa wazazi wangu, au kwa kaka zangu, wangeweza kukusaidia. Madaftari tu, au hata uniform moja, vingekurudisha shuleni. Vingefanya usitembee mitaani, bila ajira, bila chakula, bila mtu wa kukutunza.

Lakini mimi, nilikaa kimya. Nikakaa kimya kwa zaidi ya miezi miwili, nikiwa na huzuni nzito. Na siku ile ulipofariki, hukuzikwa tu mwili wako hata moyo wangu ulikufa kidogo.

Ahadi Niliyokuwekea Kaburini Mwako

Siku ile, pale niliposimama karibu na kaburi lako, nilijiwekea ahadi. Niliamua ndani ya moyo wangu:

“Sitakaa kimya tena. Kuanzia leo, mimi nitakuwa sauti kwa wale wasio na sauti.
Sitakufa nikiwa sijamwokoa hata mtoto mmoja ambaye anaweza kuwa Imma
mwingine.”

Hapo ndipo roho ya utumishi ilipoanza kunikolea. Nilipoingia kidato cha tano, nikaanza kusaidia kwa kadri ya uwezo wangu. Nilihamasisha wanafunzi wachangie vitabu, sare, na mahitaji ya shule kwa wale waliokuwa na uhitaji. Nilijifunza kuzungumza, kuongoza, na kugusa mioyo. Kila nikifanya hivi, nilikuwa naukuwaza wewe, Imma. Kila nikisaidia mtoto mmoja, nilikuwa nasema moyoni: “Huyu si Imma mwingine. Huyu sitamwacha.”

BFA: Ahadi Yangu Kwako

Nilipojiunga na Cornerstone Leadership Academy, nikapata nafasi ya kukua kiroho na kiakili. Pale ndipo nilipokutana na maono ya Builders of the Future Africa (BFA). Kwa mara nyingine, niliambiwa na moyo wangu:

“Hili ndio kusudi. Hapa ndipo unapopaswa kuwa.”

Imma, BFA kwangu haikuwa tu shirika. Ilikuwa mwitikio wa ahadi niliyokuwekea kaburini mwako. Tuliwasaidia watoto waliokuwa wanakaa nje ya geti wakiomba sabuni, penseli, au hata kipande cha mkate. Nilikuona wewe katika kila uso wa mtoto aliyeshindwa kusoma kwa sababu ya ada. Nilisikia sauti yako katika kila ombi la msaada. Nikaona sura yako katika kila kijanaaliyekosa mtu wa kumsaidia.

Nilipata nafasi ya kuongoza BFA,mpaka sasa tunafanya kazi kwenye jamii , kugusa maisha ya watu. Tumeanzisha maktaba za jamii, tunawasaidia watoto kupata bima za afya, tunafundisha elimu ya afya ya uzazi kwa vijana. Lakini zaidi ya yote, tunajenga kizazi cha vijana wanaoamini katika kutoa kwa sababu wewe ulinifundisha.

Siku moja, nilikutana na msichana mdogo aliyekuwa anaomba msaada wa ada. Niliamua kutumia akiba yangu kumpeleka shule ya bweni. Leo hii, anafanya vizuri mno. Watu wakimuona hawawezi kuamini alikotoka. Lakini mimi ninajua. Kila nikimwangalia, nakuona wewe, Imma. Naona kile ambacho ungeweza kuwa. Na najua: Sikukaa kimya tena.

Ndoto Yangu Sasa Kwa Ajili Yako

Watu wanadhani BFA ipo ili kutoa madaftari na misaada wa watoto. La hasha, Imma. BFA ipo kuamsha moyo wa utu, moyo wa matumaini. BFA ipo kuhakikisha hakuna mtoto mwingine atakayekufa mitaani kwa sababu hakuwa na mtu wa kumsaidia. Ndoto yangu ni kuona BFA

ikiwa na wanachama angalau mmoja katika kila nchi ya Afrika kama vile virusi vya upendo, vinavyoenea na kuambukiza moyo wa kujitoa.

Sina ndoto ya majengo makubwa. Lakini nina ndoto ya mioyo mikubwa. Mioyo ambayo haiwezi kukaa kimya pale mtoto mmoja anapohitaji msaada.

Nakutafuta Katika Kila Mtoto Ninayemsaidia

Imma, natumaini huko ulipo, una amani. Natumaini yale maumivu uliyopata siku ile yameshaisha. Natumaini kuna mahali ambapo watoto maskini, waliotelekezwa na jamii, wanapokea upendo na heshima wanayostahili.

Natumaini siku moja, tutakutana tena. Natumaini utanikumbuka. Na natumaini, huko ulipo, unasikia sikukaa kimya tena.

Kwa upendo, machozi, na ahadi ya milele,
Elisante Ephraim
Arusha, Tanzania

P.S. Kaburi lako bado liko Kimandolu. Ninaenda mara kwa mara. Nileta madaftari mara yakwanza nilikotembea. Niliweka pale, nikasema: “Haya ni yako, Imma. Yalikuchelewa, lakini ni yako.” Daima utakuwa rafiki yangu. Daima.

Imehaririwa na Rebecca Nyeleshi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *