Na Doricas Singano – NLF Alumni
Simu: 0763 826 912
Tarehe: 28/06/2025
Umri: Miaka 30+
Kazi: Mkaguzi wa Fedha
Makazi: Dar es Salaam
Asili: Tanzania
Nilikuwa hospitali ya mkoa wa Morogoro hivi karibuni, Nikifanya ukaguzi wa stoo ya dawa ya hospitali. Baada ya kumaliza tukawa tunatoka chumba kimoja kwenda kingine. Tumeongozana watu watatu mimi nyuma na mkaguzi mwenzangu ametangulia. Nikashangaa nimeguswa begani. Mkaguzi mwenzangu akaniambia unaitwa pale.
Kuangalia anayeniita ni rafiki yangu tuliyepotezana kwa zaidi ya Miaka 17. Leo yeye amekuwa daktari na mimi ni mkaguzi wa hesabu za fedha na nimeenda kumkagua. Machozi yalinitoka kwa Furaha. Nikawaambia na Wenzangu nipo hapa sababu ya huyu kaka. Yeye ndiye amenisaidia kwenye safari ya elimu, na mimi leo nimekuja kumkagua. Nimesoma nae toka darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Miaka yote hiyo Sikuwa na Mkalimani yeye ndio alikuwa anamsikiliza mwalimu na kunielezea na hakuwahi kuchoka wala kukataa. Huenda asingekubali nisingekuwa Doricas unamjua leo hii.
Watu wengi ukiwauliza mtu aliyechangia kwenye safari ya maisha ni nani watakujibu wazazi. Kwangu mimi ni watu wengi. Wengine hata sio ndugu wa karibu.
Nyumbani Walidhani Najifanyisha
Nilikuwa na miaka saba nilipoanza kupoteza uwezo wa kusikia. Tatizo hili lilianza baada ya kuumwa homa ya Malaria na kuchomwa sindano ya Quinine ambayo ilipelekea madhara kwenye masikio yangu. Mwanzo ilianza polepole. Nyumbani hawakuelewa nilichokuwa napitia. Nilianza kugombana na watu nyumbani na wazazi walinichapa nilipowaambia sikuwa nasikia vizuri, wao walifikiri nagoma makusudi.
Ilikuwa vigumu kuelewa walichotaka kusema. Hatimaye waligundua kuwa hata namna ya kuzungumza kwangu imebadilika na haikuwa ya kawaida. Ikawashtua sana wakahisi kuna kitu si sawa. Waliponipeleka hospital daktari akasema nimeshapoteza uwezo wa kusikia. Nimekuwa Kiziwi na ghafla dunia yangu ikabadilika kuwa kimya. Ilikuwa ngumu kuelewa dunia bila sauti, lakini nilijitahidi kuendana nayo. Niliishi kwenye dunia ya ukimya, lakini nilikuwa na ndoto.
Mpelekeni Shule ya Watoto wa Kawaida
Dunia yangu ilibadilika sana. Haikuwezekana kuendelea na shule niliyokuwa nimeanza tayari. Tukaanza safari ya kutafuta shule mpya ambayo watakubali kunipokea pamoja na changamoto yangu ya kutokusikia. Kila shule tuliyoomba walitukalia “Hatupokei Watoto Viziwi, jaribuni shule nyingine.”.
Hata Tulipoenda kwenye shule ya viziwi, mwalimu mkuu aliomba matokeo yangu, alipoyaona aliona tofauti ndani yangu. Akawaambia wazazi wangu “Mpelekeni shule ya watoto wa kawaida”. Mama yangu hakuwahi kukata tamaa. Alinipeleka kwenye shule ya msingi ya kawaida, siyo shule ya watu wenye ulemavu.
Safari Mpya ya Elimu
Nilijiunga na shule ya shirika la New Life Foundation toka darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Hapo ndipo mlango wa matumaini ulipoanza kufunguka. Tofauti na shule zingine wao, waliona uwezo badala ya ulemavu. Walinipokea kwa mikono miwili, wakanipa kiti mbele ya darasa karibu na mwalimu.
Wanasema mtu yoyote anafahamu karibu asilimia 80 za lugha ya alama. Kwa miaka yote ya elimu toka darasa la kwanza hadi chuo nimesoma shule za kawaida. Nilikuwa nikiwasiliana kwa kusoma midomo, na kuzungumza kwa alama. Nilihakikisha kila neno walilosema nalielewa kupitia usoni mwao.
Nafasi ya Juu Serikalini
Baada ya kumaliza chuo kikuu niliona tangazo la nafasi ya kazi. Nilifanya maombi na nikaitwa kwenye usaili. Ilipofika muda wa usaili wa kuzungumza, nikajiambia lazima nipambane na nikazungumza kwa ufasaha sana na wakaona uwezo wangu. Moja kwa moja nikaajiriwa kama mkaguzi wa fedha kwenye ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG). Imekuwa miaka kadhaa sasa tangu nianze kazi na sijapata changamoto yoyote. Hata wale ambao waliniangalia kwa huruma sasa wanasema: “Doricas anaweza.” Nimefanya kazi hiyo kwa miaka kadhaa sasa, nikibeba uzito wa majukumu makubwa.
Niliwafundisha wenzangu wasiokuwa na Ulemavu
Ukiniuliza “Nini kimenipa nguvu?”
Nitakujibu “Ni imani ya wazazi wangu. Wao hawakukata tamaa. Waliniamini hata pale ambapo dunia ilinikataa.”
Na mimi sikuwahi kukata tamaa. Hata darasani, wakati shule nzima walikuwa wanasikia, mimi nilikuwa peke yangu kiziwi. Lakini pamoja na hali yangu ya kutosikia nilikuwa nawafundisha wenzangu walipokuja kuomba msaada wa masomo hasa Kiingereza. Nilijua hapo kuwa mimi siyo wa kawaida. Nilikuwa na kitu cha kipekee.
Nilihamasika zaidi pale nilipogundua kuwa naweza kuwasaidia wengine kupitia uzoefu wangu. Nilianza kushiriki katika harakati mbalimbali, nikatoa mafunzo, nikahudhuria vipindi vya redio na makongamano kuhusu watu wenye ulemavu. Nilijua kuwa nilipaswa kuwa sauti ya wale ambao hawakuwa na jukwaa. Kila hatua niliyochukua ilikuwa ni daraja kwa wengine.
Mtoto Wangu Anajua Ninayopitia
Mimi ni mama nina mtoto mmoja wa kike kwa hiyo ni binti yangu. Ilichukua muda sana kwa binti yangu kunizoea na kujifunza kuzungumza na mimi kwa sababu yeye sio kiziwi. Siku moja nilikuwa na mtoto wangu kwenye taksi. Nilikuwa najaribu kuzungumza na dereva na bahati mbaya dereva hakuwa ananisikia inabidi ageuke kila muda. Ghafla mtoto wangu akanigeukia akanigusa ni kama anasema “Relax nipo hapa kwa ajili yako.” Akaniambia amesema “Mama, amesema hivi…” Alikuwa mdogo sana, miaka kama mitano, lakini alielewa changamoto ya mama yake. Hicho kilikuwa kitu cha kipekee sana. Nilipata faraja sana kujua mwanangu anajua changamoto za mama yake akiwa bado mdogo, na anaonyesha huruma na msaada wa hali ya juu.
Niliwahi kuwa kwenye uhusiano wa miaka nane. Mpenzi wangu hakuwa na mtazamo sahihi kuhusu wanawake. Alisema mwanamke hapaswi kufanya kazi, hapaswi kusimama mwenyewe. Tuligombana sana. Ilifika wakati ikabidi kuchagua kati ya mahusiano na mimi kuendelea na kazina harakati zangu. Nilijua watu wengi hasa wenye ulemavu walikuwa wakiniangalia, wakipatamoyo kupitia mimi. Nilijua nisingeweza kufa moyo. Nilichagua kuondoka kwenye mahusianohayo. Ilikuwa moja ya maamuzi magumu sana niliyowahi kufanya, lakini pia yenye manufaamakubwa.
Nilijifunza kuwa upendo wa kweli haupaswi kufifisha ndoto zako. Huo ulikuwa uamuzi wakipekee ambao umebadilisha mwelekeo wa maisha yangu. Leo hii, najivunia kuwa mwanamkemwenye msimamo, mwenye dira, na asiyeogopa kusema “hapana” pale inanibidi.
Napigania Uwakilishi na Ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu
Kila mwaka ripoti za mkaguzi wa hesabu za serikali zinaposomwa zimekuwa haziwafikii watu wenye ulemavu kama wangu. Watu wenye ulemavu wanakosa taarifa muhimu kuhusu nchi yao na wanashindwa kushirikishwa katika maamuzi mbalimbali. Lakini ikifika kwenye kodi na wao wanalipa sawa na watu wa kawaida lakini na sheria hawaiwaonei huruma, hiyo si sawa. Pembeni ya kazi yangu rasmi, najihusisha pia na harakati za kijamii, siasa, na afya hasa kwa watu wenye ulemavu.
Kwa mara ya kwanza ripoti ya mwaka huu imetafsiriwa kwa lugha ya alama naamini hii ni hatua muhimu uwakilishi wenye kina, wenye kuelewa maisha ya kila kundi maalum. Si kwa kubahatisha, bali kwa kuishi kweli hizo tofauti. Hii si zawadi , ni haki yetu.
Utambuzi wa Kimataifa na Tuzo
Kupitia harakati zangu za kutetea haki za walemavu, nimepokea tuzo mbali mbali. Sitasahau siku nilipopewa taarifa ya kuwa nimeteuliwa kupokea udaktari wa heshima. Nilishtuka sana nikamshirikisha mama yangu. Mama yangu aliniambia “Kama hautaki kupokea, basi pokea kwa ajili yetu”. Alijivunia mafanikio yangu. Sikuwa na namna ya kukataa zaidi. Mara nyingine niliitwa kwenye kwenye kongamano moja bila kujua nikakabidhiwa tuzo. Waliniita mbele, wakasema: “Huyu ndiye Malkia wa Nguvu.” Sikuamini. Walisema, “Tunakupa tuzo hii sababu ya jinsi unavyotetea wanawake, na jinsi unavyotoa kutoka moyoni, unastahili tuzo hii.” Siku hiyo nilijua kuwa dunia inaniona.
Tuzo hiyo haikuwa yangu peke yangu. Ilikuwa ya wale wote wanaotetewa nami, wale wote waliopitia kama mimi. Ilikuwa ishara kwamba sauti zetu zinasikika. Kwamba juhudi hazipotei. Kwamba unapojitoa, dunia haikusahau.
Ndoto za Mabadiliko kwa Wengine
Ningepewa nafasi ya kubadilisha maisha ya mtu, ningesaidia watoto wenye ulemavu ambao jamii imewakataa. Naona jinsi tunavyokataliwa, kama vile dunia haiko tayari kutupokea. Ningeweza, ningemsaidia ajue kuwa yeye ni wa thamani kama wengine. Mungu akinipa nafasi, nitawasaidia zaidi.
Na si kwa huruma bali kwa haki. Kwa kuwapatia elimu, kwa kuwaweka kwenye mazingira sahihi, na kwa kuwasikiliza. Nilivyopitia mimi si tofauti sana na wanavyopitia wao. Ila nilipata nafasi, nilipata mtu aliyeniamini. Sasa nataka kuwa mtu huyo kwa wengine. Nimeamua kurudi nyuma kuwavuta wengine mbele.
Mungu amenipa neema. Siishi kwa nguvu zangu, na hiyo ndiyo sababu sijakata tamaa. Maisha yangu ni ushuhuda kuwa ukikubali kuwa tofauti, unaweza kuwa nuru kwa wengine. Dunia ikitambua tofauti zetu, itakuwa bora. Ndiyo maana nasema:
“Mimi ni kiziwi, lakini dunia inanipaza sauti.”
Mhariri/Mahojiano: Aurelio Mofuga