Safari ya Njia za Panya

Jina: Johari Masele
Mzaliwa: Msewe, Dar Es Salaam
Umri: Miaka 53
Kazi: Mfanyabiashara wa Zamani.

Niliondoka nyumbani asubuhi, nikamwacha mama akinitazama kwa macho yaliyojaa hofu na matumaini. Mdogo wangu wa miezi saba nilimuaga kwa busu la haraka. Nilimwambia mama: “Naenda mbele kutafuta Maisha, labda Mungu atanibariki.” Baba yangu alikuwa ashafariki zamani, hivyo mama alinipa baraka zote akaamini labda mwanaye atarudi na maisha mazuri.

Mimi na rafiki yangu wa tangu darasa la kwanza, Seba, tulikuwa Msewe lakini shughuli zetu tulifanyia sana Tandale na Manzese, tukipambana na biashara za mitumba. Tulivumilia mpaka mwaka ‘98, Seba akasema “bana, mimi naenda South Africa.” Akaniacha, na mimi nikabaki na mawazo yangu: labda nami niondoke, hii biashara hainiletei kitu. Nilikuwa nasikia story za mtaa watu wameenda Sauzi, wengine hadi Spain na Japan. Nikajipa moyo: “Nani atakupa bila kupambana?”

Sikuwa na pesa nyingi. Nilichukua cheni na vitu vingine vichache nikaviuza Nilianza safari: Kisutu Mnazi mmoja mpaka nikaingia Mtwara, nikavuka mpaka kuingia Mozambique. Nilikuwa na rafiki ambaye kwa sasa yuko Japan, tukakutana na vijana wengine wawili kutoka Mbagala kwahyo tukawa jumla wanne na wote tukiwa na ndoto moja ya kufika Sauzi.

Hakukuwa na magari, tukatembea kwa mguu. Tulivuka pori la Namoto, masaa matano, mpaka tukafika kijiji cha Palma. Pale Kiswahili kilikuwa kinaeleweka, nikapumua kidogo. Safari ilikuwa ni kuungaunga gari hili, gari lile, kushuka na kupanda. Tulikuwa tunauza vile vitu vidogo tulivyotoka navyo nyumbani ili tupate pesa ya nauli na ya matumizi mengine madogo njiani.

Tulipofika mto Zambezi, nilisikia hofu isiyoelezeka. Ule mto ulikuwa na mamba wengi. Tukakodi mitumbwi ya wavuvi, tukavuka huku nikisali moyoni: “Mungu, nisizame.” Bahati nzuri tukafika upande wa pili, sehemu inaitwa Dondwe.

Tukiwa tunaendelea, tukakutana na mama mmoja anauza mahindi. Tulivyokuwa hatuna nauli ya kutosha, dereva akasema: “Saidieni kupakiza magunia, nitawapeleka Maputo.” Tulikubali, na tukafika Maputo mchana wa kesho yake. Hatujui mtu yeyote, hatuna pa kuanzia.

Tukaambiwa nendeni Shamanulu, mtakutana na Watanzania. Tulifika na kweli tukawakuta. Wakatuonyesha njia ya kwenda South Africa: porini, njia za panya. Tulifika mpaka boda jioni saa kumi na moja. Hatukuwa na pasipoti kubwa tulikuwa na temporari passport ambazo hazigongwi mihuri. Jamaa mmoja akatuambia, “Usiende hivyo, mtakamatwa. Kuna njia za panya, lakini inabidi muwe makini maana kuna ulinzi mkali.

Tukanyanyua nyavu sehemu moja iliyokatwa kwenye uzio, patrol ilikuwa inapita kila wakati, moyo ukipiga mwendo kasi, lakini hatimaye tukafanikiwa kuingia kijiji cha kwanza South Africa kinachoitwa Manguzi. Huko watu waliongea Kizulu tu, hatuelewi kitu.

Basi tuliamua kwamba kwa maana tumeshafanikiwa kuingia sehemu ambayo tulikua tunaitaka, kila mtu afuate njia yake aende kupambana mbele kwa mbele maana tuliona kukaa wote wanne kwa pamoja ni rahisi kukamatwa. Basi tukaagana pale, tukatakiana kila la kheri na kila mtu akashika njia yake. Mimi nilitembea bila kuelewa naenda wapi lakini kwa bahati nzuri nilifanikiwa kupata hifadhi kwa familia moja ya Kizulu. Niliwaeleza kwamba ndoto yangu ni kwenda Durban lakini sijui namna ya kufika pale na pia sina pesa. Basi tukakubaliana kwamba niwasaidie kazi zao za nyumbani alafu watanilipa. Nilifanya hivo na baada ya mwezi walinipa rand 500. Nikaondoka pale, nikapanda basi mpaka Richards Bay. Hapo nilikutana na Msomali mmoja aliyewahi kuishi Tanzania na alinielekeza bandarini sehemu ambapo Watanzania wengi wapo na wanajishughulisha na shughuli mbali mbali ambazo kidogo zinalipa.

Basi nilipofika pale nilikutana na watanzania wengi na walinipokea vizur, nikifanya kazi mbalimbali za mikono. Lakini ndoto yangu bado ilikuwa ni kufika Durban. Baada ya kukusanya pesa kidogo nilipanda gari, nikafika Durban, Kwazulu Natal. Nilipata kazi ya kubeba mizigo bandarini. Baada ya kukaa kwa miezi mitano pale niliamua sasa kujaribu bahati yangu ya kuzamia meli ili niende ulaya. Basi nilijipanga na mwisho wa siku nikazamia meli moja iliyokua inaelekea Italy, nilijificha chumba cha injini. Lakini siku ya ukaguzi meli ikiwa safarini, walinikamata na walitaka kunirusha kwenye maji, niliomba sana wasinifanyie hivo, walikubali na badala yake wakaniambia tutakuacha Cape Town.

Basi niliamua kubaki pale Cape Town nitafute maisha pale maana niliona kama sina bahati ya kwenda Ulaya. Nilikaa pale kwa zaidi ya miaka 20, nilifanya kazi nikapata familia mke na watoto wawili. Lakini bahati mbaya pia nikajikuta kwenye njia mbaya. Mwaka 2019, mimi na wenzangu wawili tukavamia nyumba ya watu kuiba. Tulikubaliana mi niingie kutoa vitu wakati wao wanaangalia usalama wa nje. Basi walipotugundua wenzangu walikimbia, mimi nikabaki basement nikakamatwa. Nilipelekwa mahakamani na kuhukumiwa miaka mitatu jela Tokai.

Mwaka 2023 nilipotoka, serikali ya South Africa ilinipa tiketi moja kwa moja kunirudisha Tanzania. Sikupewa muda hata wa kuwaaga familia. Niliachwa uwanja wa ndege, na pesa kidogo tu ya nauli. Nilifika Dar, nikakodi boda kunirudisha nyumbani Msewe.Saivi naongea na mke na watoto kwa simu. Wananiuliza: “Baba, utarudi lini?” Natamani nirudi, lakini sitaki tena njia za panya kama zamani. Nataka nikae, nitafute vibali vya kweli, nirudi kuwaona kisheria.

Nimeishi porini, nimevuka mito yenye mamba, nimekamatwa, nimefungwa, lakini bado moyo wangu una ndoto. Hii dunia ya panya inanifunza kuna wakati lazima usimame, utafute njia halali.

Pengine siku moja nitarudi. Pengine sitarudi. Lakini moyo wangu uko na familia yangu na safari yangu bado haijaisha.

Mhariri/Mahojiano na: Primi F Fidelis

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *