Na Mary Nicas Manya
Umri: Miaka 33
Kazi: Mtawa wa kike
Makazi: Ubungo Msewe, Dar Es Salaam
Asili: Tabora / Dar Es Salaam
“Sisi watoto wa professor”
“Baba yangu alikuwa profesa. Alijua lugha zaidi ya kumi. Alifundisha Kiswahili Chuo Kikuu. Alizawadiwa na Waziri Mkuu kwa mchango wake. Tulikuwa na maisha ya kifalme. Lakini leo, tunaishi kwa neema ya Mungu na msimamo wetu tu.”
Nilizaliwa kwenye familia ambayo kwa kweli ilijengwa juu ya misingi ya wema, upendo na heshima. Tuliishi maisha mazuri kwa kila kipimo. Tulikuwa na kila kitu: chakula cha uhakika, nyumba ya kifamilia, na wageni wa kila aina. Wageni wa ndani na wa nje ya nchi walikuwa wanakuja baba, alikuwa Meneja wa Estate Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikabidhiwa nyumba za wageni wa kigeni, na alipenda sana kusaidia.
Baba hakutaka tu tuishi kwa anasa. Alituonyesha pia maisha ya upande wa pili akatupeleka shamba, akatufundisha kupika kwa kuni, kutumia mkaa hata kama gesi ipo. “Ni lazima muelewe maisha yote,” alisema.
Kila mtu alikuwa anasaidiwa. Wageni zaidi ya kumi walikuwa wanaishi nasi. Wengine kutoka upande wa mama, wengine wa baba. Waliopata kazi, waliopata kwenda kuishi Ulaya, waliopata elimu wote walipitia nyumbani kwetu. Hata Mama Gertrude Mongella, ambaye ni shangazi yetu, aliwahi kujifunza maisha ya chini kutoka kwa baba na kwenda kuwafundisha watoto wake, hata alipokuwa Mbunge.
Lakini ilipofika wakati baba ametoka kazini, mambo yakaanza kubadilika. Tulianza kuona watu wakipungua Wakipotea Wale waliokuwa karibu kila siku hawakuonekana tena.
Kama hilo halikutosha, tukakumbana na kisanga kingine kibaya zaidi.
“Walitaka kutunyang’anya ardhi yetu”
Wavamizi walivamia eneo letu la familia Baba wakati huo alikuwa mzee, macho hayamuoni vizuri. Walimrubuni sio kwamba aliwauzia, la hasha. Bali walimuandama kwa hila, wakitumia hata ushirikina na rushwa.
Mtu wa serikali za mitaa akishirikiana na mwanasheria mmoja ambaye hadi leo jina lake linatutia hofu Walitaka kutupora eneo letu lote. Tulipokataa, wakasema, “Tutaliuza lote.” Wakaanza kutumia silaha Risasi zikaanza kulia Waliamua kututisha watoto wa mzee. Ilikuwa vita ya kisaikolojia na kimwili.
Kaka yangu alifyatuliwa risasi na mtu mmoja anayejiita usalama wa taifa. Walimlenga kichwani, akakwepa, lakini risasi tatu zikampata tumboni Tukampeleka Mwananyamala, kisha Muhimbili. Bahati mbaya kipindi hicho kulikuwa na mgomo wa madaktari (mgomo wa Ulimboka). Ilibidi ndugu zetu wapige simu kila kona hadi tukapata daktari kutoka Aga Khan, akaja kufanya upasuaji. Walimwokoa Hadi leo ana mshono tumboni.
Kesi iliandaliwa haraka dhidi yetu, wakadai kaka aliwatishia kwa mapanga Polisi walikuwa wanatumika kutukandamiza. Tulikuwa tukilala na kufunga milango hata mchana Usiku tunasali, asubuhi tunashukuru kwa kuwa hai.
Tulifikisha barua zetu hadi kwa Rais. Ndipo walipoanza kuchunguza Polisi wakaambiwa wasisogee tena kwa familia yetu. Ndipo tulianza kupata amani, pia watu waliokuwa pamoja nasi sio ndugu waliowahi kuishi nasi bali watu baki pia Padri mmoja alitusimamia kiroho hadi kifo chake. Watu wa mbali walitushika mkono, si wale tuliowahifadhi kwenye nyumba yetu miaka yote.
“Nilijifunza kitu kimoja kikubwa: usiweke tumaini lako kwa wanadamu.”
Kuna kipindi ndugu yetu mmoja aliwahi kutuuliza, “Hawa wote mnaowapa msaada, watakuja kuwsaidia siku moja?” Mama alimjibu kwa utulivu, “Tenda wema uende zako.” Hilo lilikaa moyoni mwangu hadi leo. Nilijifunza kutenda wema bila matarajio.
Sasa nina msimamo. Mimi ni mimi. Sina muda wa kujipendekeza kwa watu, Rafiki wa kweli kwangu ni mtu aliyenyooka Sitaki uongo Sitaki unafiki. Nimejifunza kupitia risasi, mapambano ya ardhi, na usaliti wa damu yangu mwenyewe. Hadi leo, wengine wanasema hawahitaji kuwa na watu na ni kweli.Dada zangu, kaka zangu, walikua ndani ya maumivu haya.
Nilipata nafasi ya kwenda hadi Spain, Nikarudi kwa ajili ya familia yangu. Maisha hayakuwa mepesi, lakini Mungu alitupigania. Tulijifundisha kupigana wenyewe. Leo hii bado tunaishi kwenye nyumba ya baba, imechoka, lakini ni ya kwetu Na hatuondoki.Tulizaliwa hapa, tutafia hapa.
“Baba yangu alisaidia watu wengi lakini walimsahau. Mimi sitasahau. Nitajenga kwa msimamo wangu, kwa jasho langu, na kwa imani yangu.”
Mhariri/Mahojiano na: Neema Mikomangwa,